Mvua nyepesi ilikuwa ikiendelea kunyesha mjini Mombasa usiku huo. Barabara nyingi zilikuwa kimya huku upepo wa bahari ukivuma kwa sauti ya kutisha. Saa ilikuwa imekaribia saa sita usiku wakati Amani aliposhuka kwenye basi la mwisho kutoka kazini.
Alitembea haraka huku amevaa hoodie yake nyeusi, akijaribu kujikinga na baridi. Simu yake ilikuwa na asilimia tano tu ya betri. Kitu pekee alichotaka ilikuwa kufika nyumbani, kuoga, kisha kulala.
Lakini alipofika karibu na kona ya mtaa wao, simu yake ilianza kuita.
Namba haikuwa imehifadhiwa.
UNKNOWN CALLER.
Amani alisita kwa sekunde kadhaa. Kwa kawaida hakuwahi kupokea simu za watu asiowajua usiku. Mara nyingi zilikuwa prank calls au watu waliokosea namba.
Simu iliendelea kuita.
Mwishowe akaipokea.
“Hello?” alisema kwa sauti ya uchovu.
Hakukuwa na jibu.
Kimya kizito kilitawala kwa sekunde chache.
Kisha sauti ya mwanamke ikasikika kwa mbali, ikiwa ya chini na yenye hofu.
“Amani… usiende nyumbani leo.”
Mwili wake ulisisimka ghafla.
“Nani huyo?” aliuliza haraka huku akisimama kutazama nyuma yake.
Lakini simu ikakatwa.
Amani alibaki amesimama katikati ya barabara akiwa amechanganyikiwa. Aliangalia tena screen ya simu yake lakini bado ilikuwa UNKNOWN NUMBER.
“Watu wana mchezo mingi sana,” alijisemea huku akianza kutembea tena.
Dakika moja baadaye, simu yake ikatoa notification nyingine.
MESSAGE RECEIVED.
Akiwa na wasiwasi, aliifungua haraka.
«UKIFIKA NYUMBANI… UTAJUTA.»
Mapigo ya moyo wake yakaanza kwenda kasi.
Safari hii hakucheka.
Aliangalia pande zote za barabara. Hakukuwa na mtu. Taa za mtaa zilikuwa zinawaka hafifu huku mbwa wakibweka kwa mbali.
Amani alianza kuhisi kama kuna mtu alikuwa akimfuatilia.
Aliongeza mwendo.
Baada ya dakika chache alifika mbele ya nyumba yake.
Na hapo ndipo aliganda.
Mlango ulikuwa wazi kidogo.
Kitu ambacho hakikuwa kawaida.
Amani alikuwa anaishi peke yake.
Polepole alisogea karibu na mlango huku moyo wake ukidunda kwa nguvu. Alisukuma mlango taratibu.
“Kuna mtu?” aliita.
Hakuna aliyemjibu.
Ndani kulikuwa kimya sana.
Kimya cha kutisha.
Alitoa simu yake na kuwasha flashlight. Sebule ilikuwa giza tupu.
Lakini alipiga hatua moja mbele, mguu wake ukakanyaga kitu laini.
Alipoangaza chini…
aliona damu.
Damu ilikuwa imetapakaa sakafuni kuelekea upande wa jikoni.
Mikono yake ilianza kutetemeka.
Ghafla akaona kitu kingine ukutani.
Kulikuwa na ujumbe ulioandikwa kwa damu:
«UMEANZA KUCHELEWA.»
Amani akarudi nyuma kwa hofu.
Na ghafla mlango wa nyuma ukafungwa kwa kishindo kikubwa.
BWAAAM!
Macho yake yakapanuka kwa woga.
Kisha sauti nzito ya mwanaume ikasikika gizani nyuma yake.
“Hatimaye umerudi…”